UINJILISHAJI RASMI WA ENEO LA UPARE

Mwanzoni mwa Karne ya 20, eneo la Upare lilishafikiwa na madhehebu ya Kiprotestanti na Kisabato. Mmisionari wa kwanza wa Kilutheri kufika alikuwa ni Mchungaji Hans Fuchs ambaye alisimika hema lake Julai 11, 1900 katika eneo la Shighatini (Usangi), Pare kaskazini. Alifuatiwa na Mchungaji Jakob Jansen Dann Holz mwaka 1907 ambaye alihamia Mbaga (Pare Kusini) mwaka 1908. Mwaka 1903, Wasabato walikuwa wameshajikita Bwambo (kusini milimani) katika eneo la Giti (ambalo Wajerumani waliliita Friedenstal ) na baadaye wakaweka maskani eneo la Suji.

Kilomeni, iliyoanzishwa mwaka 1909 kama misheni ya kwanza ya Kikatoliki Upareni, ina historia yake ya kuvutia ambayo ndiyo iliyoandaa uwanda wa kusia mbegu ya kwanza ya uinjilishaji. Enzi hizo (mwishoni mwa karne ya 19) za njaa kuu ya mnyime wakati makabila jirani yalikuwa yakiivamia Pare kuiba mazao na wanyama, watu toka Taita (Kenya) walishambulia Kilomeni na kuondoka na vijana wanne waitwao Shengena Kasira na dada yake aliyeitwa Nangida, Kompeho Ngosari na Kichawele Mashengere. Bahati nzuri wakiwa Taveta (Kenya), Shengena, Kompeho na Kichawele, walikombolewa na wamisionari wakapelekwa misheni ya Bura, wakafunzwa dini, kuandika, kusoma pamoja stadi za ujenzi na kazi za mikono na hatimaye wakabatizwa Aprili 5, 1895 kwa majina ya Ignasi, Victoria na Lusia. Aprili 22, 1901, Ignatius Shengena, akamwoa Victoria Kompeho, na familia ndiyo ilikuja kuwa chanzo cha kuletwa dini ya kikatoliki Upareni.

Ignasi hakutegemea kurudi Upare, ila kwa bahati Mfumwa Kivwasi Mjewa wa Lembeni alipeleleza akajua walipo, hivyo wakamtuma Mchago Mngofi aende Bura, akawakuta tayari wana mtoto (Joakimu). Walirudishwa Kilomeni mwaka 1902 na hatimaye mwaka 1907 wakahamia kabisa Kilomeni kwani mtoto wao wa pili Francis alizaliwa Kilomeni na kubatizwa Januari 1908 katika misheni ya Kilema. Waliwashawishi mapadre wa Kilema kuja kuinjilisha Kilomeni, na hatimaye Askofu F.X. Vogt akaamua kuanzishwa Misheni ya Kilomeni.
Pd. Alphonse Balthazar, ndiye alipewa jukumu la kuanzisha misheni ya Kilomeni mwaka 1909. Alizaliwa Februari 2, 1878 huko Alsace, na akapadrishwa Oktoba 6, 1901 na kutumwa Afrika Mashariki mwaka 1902 na kupangwa misheni ya Kilema. Inasemekana Pd. Balthazari, alikuwa na matatizo ya macho alipokuwa akisoma seminari, akaomba na kuahidi kuwa endapo angepona, misheni ambayo angeianzisha, angeiweka chini ya usimamizi wa Mtakatifu Odilia aliyekuwa kipofu ila akapona siku alipobatizwa. Hivyo sawa na ahadi yake, aliiweka misheni ya Kilomeni chini ya usimamizi wa Mt. Odilia. Askofu Vogt alimtuma pia Pd George Metzler Kilomeni ambaye mwaka 1913 alihamia Pare ya kusini kuandaa misheni mpya ya Kwizu (1914).

Baada ya miaka mitatu ya kazi nzito ya kufundisha dini na maadili, kuandika na kusoma, ufundi-stadi, ujenzi wa mawe/matofali n.k., hapo Kilomeni, wakatekumeni 12 wa kwanza walibatizwa na Pd. Metzler Krismas ya mwaka 1911, nao ni Alfonse Kitunga, Aloice Kagulu, Andrea Mwakera, August Kihuji, Francis Nahae, Ignatius Luvigho, Laurenti Kizigha, Ludovick Tuyoye, Paul Mkichwe, Peter Semhuja, Stanslaus Nzughi na John Seishika. Walipewa kipaimara Machi 3, 1912 na Askofu Joseph Munsch, aliyekuwa Mtawala wa Kitume wa Vikarieti mpya ya Kilimanjaro.

Vita kuu ya kwanza ya dunia mwaka 1914 ilizorotesha uinjiishaji ikaleta pigo kubwa kwa Vikarieti. Pia vifo vya Pd. Balthazari (Novemba 30, 1918) na Br. Polycarp Dohmen (Desemba 2, 1918) vilizorotesha uinjilishaji kiasi kwamba kuna wakati ilibidi Kilomeni ihudumiwe kama kigango cha Kilema. Kwa kweli baada ya kuanzisha misheni ya Kilomeni mwaka 1909 na ya Kwizu mwaka 1914, hakukuwa na ufunguzi wa misheni nyingine hadi 1958 ile ya Gonja ilipoanzishwa na kufuatiwa na ya Mamba (Bwambo) mwaka 1960. Hali hii ilileta hisia kwa wakazi wa Upareni ya kuona kwamba wanasahaulika hata kwenye eneo la imani.

Kiuongozi, kwa vile Ask. Musch aliwekwa kizuizini Tanga wakati wa vita kuu ya kwanza, nafasi yake ilichukuliwa na Ask. Henry A. Gogarty (1924-1931), akifuatiwa na Ask. Joseph Byrne mwaka 1933. Mwaka 1953, Vikarieti (majimbo machanga) zote ziligeuzwa kuwa Majimbo kamili ( regular dioceses ) (yaani ya kawaida . Hivyo, Zanzibar ikahamia kuwa Jimbo Kuu la Nairobi, Bagamoyo ikawa Jimbo la Morogoro, na Kilimanjaro ikawa Jimbo la Moshi. Dodoma ambayo ilishakuwa Prefecture tangu 1935 na Vikarieti mwaka 1952 ikawa Jimbo mwaka 1953. Pia Mbulu iliyokuwa Prefecture mwaka 1943 ikawa Jimbo mwaka 1953, na Tanga ambayo ilifanywa Prefecture mwaka 1950 ikawa Jimbo mwaka 1958.
Hivyo, Machi 25, 1953, Mhashamu Byrne alisimikwa rasmi kama Askofu kamili wa Jimbo la Moshi, ikiwa ni eneo lote la Kilimanjaro (Moshi na Pare) na Arusha. Mwaka 1959 Askofu Byrne alijiuzulu, ndipo mwaka 1960, Pd. Joseph Placide Kilasara (C.S.Sp.) akateuliwa kuwa Askofu mwafrika wa kwanza kuongoza Jimbo Katoliki la Moshi. Kutokana na ukubwa wa jimbo hilo, Papa Yohane XXIII aliridhia kuligawanya likazaliwa Jimbo la Arusha (Machi 1, 1963) na eneo la Pare likatangazwa kuwa Prefecture ya Same, Desemba 10, 1963.

Hakika uinjilishaji wa maeneo ya Jimbo la Same ulikuwa moja ya safari ndefu iliyokuwa imejaa majitoleo mengi na hatimaye kuzaa mafanikio na matunda yaliyojaa neema ya Mungu, na ni matunda yaliyotokana na misingi iliyotolewa jasho na wamisionari kwa kushirikiana na waamini wa kwanza katika maeneo ya Upareni, hasa wale wa eneo la Kilomeni.

MAENDELEO YA PREFECTURE YA SAME

Mhashamu Joseph Kilasara C.S.Sp. alipoteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Moshi, eneo la Upare lilikuwa na misheni nne tu, yaani Kilomeni (1909), Kwizu (1914), Gonja (1958) na Mamba (1960), na kati ya mapadre wazalendo 40, wanne tu ndiyo walikuwa wenyeji wa Upare, yaani Pd. Andrew Kivaria aliyepadrishwa mwaka 1944, Pd. Leonard Kiure aliyepadrishwa 1951 na Mapadri Phocas Abed na Sabas Msuya waliopadrishwa mwaka 1961.

Prefecture ya Same ilipoundwa Desemba 10, 1963 ilibidi kuongezwe mapadri wengi wamisionari. Hivyo kundi la mapadri Waholanzi wa Shirika la Roho Mtakatifu toka Jimbo la Morogoro walihamishiwa Same. Miongoni mwao, alikuwapo Pd. Henry Winkelmolen ambaye Januari 3, 1964 aliteuliwa kuwa Msimamizi ( Prefect ) wa Kitume wa Prefecture ya Same. La kushangaza ni kwamba waumini wa Same walizoea kuiita Prefecture yao Jimbo, na Monsinyori Henri walimwita Askofu!

Kazi ya kwanza Same ilikuwa ni kuimarisha uinjilishaji, uchungaji na kuanzisha misheni mpya. Hivyo, Same iliyokuwa na makazi madogo tu, na kuhudumiwa toka misheni ya Kwizu, ilipandishwa hadhi mwaka 1964 kuwa misheni (Parokia) na makao makuu (makazi) ya Msimamizi wa Kitume wa Prefecture mpya ya Same. Pia misheni ya Msindo (Chabaru) iliyokuwa ikihudumiwa toka Gonja, ilifunguliwa mwaka 1964, ikafuatiwa na ya Ugweno (1965). Mwaka 1966, misheni za Kisangara Juu na Kisiwani zilianzishwa zikafuatiwa na misheni za Chanjale na Lembeni (1969). Sasa hali ikawa inaruhusu kuandaa programu za kichungaji kwa ajili ya Prefecture ya Same, na mojawapo mahususi ilikuwa semina ya Kwizu (1968) kwa ajili ya utekelezaji wa maamuzi ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano hasa kuhusu utume wa walei. Desemba 11, 1968 ukafanyika upadrisho (wa kwanza tangu Prefecture ianze) wa Josaphat L. Lebulu uliotolewa na Ask. Dennis Durning wa Arusha.

Mwaka 1972, Prefecture ya Same ilikuwa na Parokia 11 wakati Tanzania nzima ilikuwa na majimbo 24, zikijumlishwa na Prefecture za Same na Zanzibar.
 
Mwanzoni mwa 1974 Kanisa kuu lililojengwa eneo la Same mjini lilibarikiwa. Julai 3, 1974 Rev. Beda Ishika alipadrishwa na Ask. Joseph Kilasara na mwaka 1976, mapadri Albert/Beati Msuya na Vincent Mrema walipadrishwa na Ask. Kilasara.

Padri L. Kiure (RIP) ambaye alikuwa Makamu Prefekti wa Jimbo, alifariki Februari 1979.

UUNDWAJI RASMI WA JIMBO KATOLIKI LA SAME NA MIPANGO YAKE

Februari 3, 1977 Papa Paulo VI aliipandisha hadhi Prefecture ya Same kuwa Jimbo kamili na Monsinyori Henry Winkelmolen, aliyekuwa Msimamizi wa kitume wa Same akaendelea kama Mtawala wa Jimbo hilo hadi mwanzoni mwa 1979 alipomwachia Askofu mpya.

Awamu ya Askofu Josaphat L. Lebulu 1979 - 1999

Mnamo Februari 12,1979, Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, alimteua Padri Josephat Louis Lebulu kuwa Askofu wa Kwanza wa Jimbo Katoliki la Same.

Mhashamu Lebulu aliyezaliwa Juni 13, 1942 na kupewa Daraja ya Upadri Desemba 11, 1968, aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Miito na Utume wa Walei. Alipewa Uaskofu Mei 24, 1979 jimboni Same. Wakati huo Jimbo lilikuwa na parokia 11 tu, mapadre wazalendo sita na wamisionari nane, pamoja na makatekista 30.

Tangu mwaka 1969, mkazo mkubwa uliwekwa katika uundaji programu yenye muelekeo katika uchungaji. Mwaka 1980, mkazo ulihamia katika uhamasishaji wa kimisionari kuanzia kwenye shina (jumuiya) kupitia ngazi za parokia, jimbo hadi ngazi ya kitaifa.

Kama mpango wa muda mrefu wa kuziba tatizo kubwa la ukosefu wa wahudumu wa kutosha, Chuo cha Malezi ya Miito kilianzishwa Chabaru mwaka 1980, baadaye kikahamia Chanjale, ndiyo Chanjale Seminari. Seminari hiyo hutoa malezi ya miito mbalimbali, yaani uongozi wa Kanisa ili kukidhi siyo tu hitaji la miito ya kipadri, bali pia miito ya utawa na hata ya kilei. Mwaka 1980, ulitangazwa kuwa wa miito kijimbo na Padri Colman Ngula alipadrishwa Juni 19, kama padri wa kwanza tangu kuundwa kwa Jimbo na pia wa kwanza kutoka Kilomeni (parokia mama iliyokuwa na miaka 71).

Upande wa Maendeleo, idara za Afya, (mfano uanzishaji wa Kituo cha Afya Bwambo, 1982) Timu ya Maendeleo (CDP), WAWATA, WDP (Hosteli ya Akinamama ilianzwa 1985), na pia Sekondari ya Kindoroko ilijengwa, Kitivo cha Ushenga (Catechetical Centre) Chabaru 1986.

Upadrisho wa Pd Kimbwe Julai 3, 1986. Mwaka 1987 Balozi wa Papa Tanzania Ask. Mkuu Vincenzo Moreini alifanya ziara ya kichungaji Jimboni. Mashemasi Jacob Koda na Valence Mruma walipadrishwa Kilomeni Juni 25, 1987. Upadrisho wa Herment Msoffe, Joseph Mlacha na Novatus Mrighwa ulifanyika Kisangara Juu Juni 23, 1988. Mwaka huo Askofu J. Lebulu alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania (nafasi aliyoishika kwa awamu mbili).

Kufikia mwaka 1988, idadi ya mapadri wa jimbo ilifikia 14. Pia kama matunda ya Chuo cha Malezi ya Miito Chanjale, wasichana kadhaa walijiunga na utawa (hasa Dada Wadogo wa Mt. Francis wa Asisi wenye makao yao Uganda na Kenya) na pia makatekista na viongozi wengine walianza kuchipua, na hata shirika la Watawa wa Kiume ( Brothers ) la Kristu Mchungaji Mwema liliweza kuanzishwa Chanjale, Same na sasa makao yake ni Hedaru.

Askofu Lebulu alitangaza Sinodi ya kwanza ya Jimbo la Same na kuadhimishwa tangu Novemba1988 hadi Agosti 1991: Kituo cha Uchungaji na Maendeleo ya Watu. Juni 14, 1989 kukafanyika Upadrisho wa Samweli Lawena na jubilee ya miaka 80 ya parokia mama ya Kilomeni. Papa Yohane Paulo II alitembelea Tanzania 1-5 Septemba 1990 na kutoa upadrisho Septemba 2 wakiwemo Bruno Chelangwa na Michael Shayo wa Jimbo la Same. Pia alibariki jiwe la msingi la kituo cha uchungaji na maendeleo ya watu. Hayo yote yalikuwa matukio ndani ya kipindi cha sinodi ya jimbo. Sinodi nzima ilikuwa na mikesha (mikutano) nane, ambamo mada 29 zilitolewa na kujadiliwa, yakatolewa mapendekezo 226 na hatimaye njozi, mbinu na mikakati ikawekwa. Kilele cha Sinodi kikawa kufungua chombo, yaani Kituo cha Uchungaji na Maendeleo ya Watu kilifunguliwa Agosti 23, 1991 ambamo timu nzima ya uongozi ingeratibishwa. Njozi kuu ya Sinodi ilikuwa: Tuwe Kanisa Analotutaka Kristo Tuwe, ikiongozwa na Neno: “Tazama Nafanya yote kuwa mapya” (Ufu 21:5)

Kanisa kuu la Jimbo Kristo Mchungaji mwema liliwekwa wakfu Mei 24, 1994.

Pd. Andrea Kivaria aliadhimisha jubilee ya miaka 50 ya upadre Lembeni.
 
Parokia mpya zilifunguliwa zilizofunguliwa katika awamu hii ni Dido (1982), Mwanga (1986), Ngulu (1989), Hedaru (1990), na Usangi (1991).

Julai 1997 Ask. Josaphat Lebulu alihamishwa kuwa Askofu wa Jimbo la Arusha (na hapo hapo Msimamizi wa Jimbo la Same) na alisimikwa Arusha Januari 31, 1998

AWAMU YA ASKOFU JACOB VENANCE KODA 1999 - 2009

Machi 24, 1999 Pd. Jacob Venance Koda aliteuliwa na Papa Yohane Paulo II kuwa Askofu wa Same, na alipewa uaskofu na kusimikwa Same Mei 30, 1999. Kadhalika tarehe hiyo ya 24 Machi Arusha ilipandishwa hadhi kuwa Jimbo Kuu na Mhashamu Lebulu akawa askofu mkuu wa kwanza.

Msisitizo: Uinjilishaji na Maendeleo ya watu. Msisitizo mkubwa uliwekwa kwenye elimu, ukombozi wa maskini na uimarishaji wa uchumi, kutunza mazingira n.k.
Katika mengi aliyofanya Mhashamu Koda, tunataja yafuatayo:

Aliimarisha na kuboresha Seminari ndogo ya Chanjale (ikiwa ni pamoja na majengo ya kisasa).

Alisisitizia sana elimu na hasa kumkomboa mwanamke. Hivyo zilianzishwa sekondari za wasichana za Kandoto na baadaye ya Mother Teresa of Culcuta. Kwa sasa pia Sekondari za Kindoroko na Kilomeni ni za wasichana. Sambamba na juhudi hizo, mashirika ya kitawa yameanzisha shule za ngazi mbalimbali katika baadhi ya maeneo jimboni.

Warsha ya uhifadhi wa mazingira hasa misitu, ardhi na maji ( Aforestation, soil and water Conservation master plan 2004-2024 ) ilifanyika Same tarehe za 19-21 Novemba 2003.

Elimu ya juu: Tarehe 06 Juni 2007 kulifanyika kikao cha ufafanuzi wa pendekezo la kujenga Chuo Kikuu cha Jimbo Katoliki la Same ( Concept Paper for Proposed University = Ngalakeri International Universit y ) na mikakati muhimu iliwekwa.

Kama ishara ya Jubilee kuu ya 2000 msisitizo uliwekwa kwenye kuwatuma mapadri wengi kwenye masomo ya juu. Kiasi cha mapadri 30 hivi walienda masomoni, na wengine walifuata kozi fupi katika vyuo mbalimbali.

Pia parokia mpya zilifunguliwa: Njoro (2007), Vumari (2008), Sonkana (2008), Myombo (2008), Ndungu (2008), Vudee Juu (2008), Makanya (2008), Kirongwe (2008), Kirangare (2008) na Dimbwi (2008) ikihusisha vigango vyote pembeni mwa bwawa la Nyumba ya Mungu.

Maandalizi ya Jubilee ya Miaka 100 ya Uinjilishaji jimboni Same: Kwa njia ya sala, semina na uhamasishaji mbalimbali, maandalizi yalianza mapema, ikiwa ni pamoja na kuboresha hali za maparokia na vigango vyake. Vituo vya hija

Maadhimisho rasmi ya mwaka wa jubilee yalifunguliwa tarehe 12 Desemba 2008 (kama vijilia ya sikukuu ya Mt. Odilia somo wa parokia ya Kilomeni) kwa maandamano ya msalaba wa jubilee toka kanisa kuu la Jimbo hadi Kisekibaha (Grail) na ikaanza hija ya kupanda mlima kwa miguu kupitia njia ya msalaba iliyojengwa zamani kabla ya uhuru, njia ambayo wamisionari waliitumia sana kufika Kilomeni. Kuanzia Kilomeni msalaba wa jubilee ulizunguka parokia na vigango vyote vya Jimbo kuchochea na kuimarisha imani. Zoezi hilo likiendelea, ndipo yalipotokea mabadiliko ya uongozi jimboni, lakini hata hivyo matendo ya kiroho na hija mbalimbali za kijubilee ziliendelea.

Juni 4, 2009 Balozi wa Baba Mtakatifu Tanzania alitangaza kuwa Mhesh. Pd. Rogath F. Kimaryo (C.S.Sp.) wa Shirika la Roho Mtakatifu ameteuliwa kuwa Msimamizi wa Kitume wa Jimbo la Same.

Alianza kazi mara moja, na kuendeleza mikakati ya maadhimisho ya jubilee iliyokuweko. Kwa parokia mama ya Kilomeni, maadhimisho ya miaka 100 ya uinjilishaji yalifanyika katika sikukuu ya Mt. Odilia, Jumapili ya tarehe 13 Desemba 2009 na kuongozwa na Askofu Beatus Kinyaiya wa Mbulu. Sherehe zilifana sana, kanisa mama likiwa limekarabatiwa vizuri sana, grotto ya Bikira Maria ikiwa imekarabatiwa na kujengewa kikanisa, na Mnara wa kengele sasa umejengwa.

Mipangilio ya kuadhimisha jubilee kijimbo ikawekwa pamoja na vipindi mbalimbali vya mazoezi ya kiroho, tarajio likiwa iadhimishwe Desemba 16, 2010.

Aprili 15, 2010 Balozi wa Baba Mtakatifu Tanzania alitangaza kuwa Papa Benedikti XVI amemkubalia Mhashamu Jacob Venance Koda kujiuzulu kama Askofu wa Jimbo la Same.
Aprili 30, 2010 Papa Benedikti XVI alimteua Mheshimiwa sana Pd. Rogath F. Kimaryo kuwa Askofu wa Same kuchukua nafasi iliyoachwa wazi baada ya Ask. Koda kujiuzulu.
Ikaonekana ni vyema kuunganisha sherehe za uaskofu na maadhimisho ya jubilee ya miaka 100 ya uinjilishaji kijimbo.

Juni 13, 2010 Mhash. Rogath F. Kimaryo C.S.Sp. kupewa daraja la Uaskofu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Same pamoja na maadhimisho ya jubilee ya miaka 100 ya uinjilishaji.

AWAMU YA AKOFU ROGATH KIMAYO

Mhashamu Rogath F. Kimaryo alizaliwa 30.10.1956 Mkuu-Rombo Moshi. Wazazi wake ni Anthoni Fundimoya na Mariana Mkolie. Alisoma shule ya msingi Ubaa, kisha akajiunga na seminari ndogo ya Maua 1973-6 na baadaye akasoma sekondari ya Mzumbe kwa kidato cha tano na sita 1977-78. Alijiunga na Jeshi la kujenga Taifa 1979. Mwaka 1980-82 alifanya masomo ya Falsafa katika seminari kuu ya Kibosho. Kisha alijiunga na novisiati ya shirika la Roho Mtakatifu huko Magamba Lushoto ambapo aliweka nadhiri zake za utawa mnamo 30.09.1983 Lang'ata Nairobi. Alisoma Teolojia katika seminari kuu ya Mt. Thomas Aquino Nairobi na kupewa daraja la Upadre mnamo Mei 30, 1987 Arusha. Aliendelea na masomo ya juu katika fani ya sheria za Kanisa Roma ( Gregorian University ) na kisha kusomea Teolojia ya uchungaji (Pastoral theology) chuo kikuu cha Leuven (Ubeljiji). Amewahi kuwa mlezi na mwalimu katika chuo cha Tangaza college Nairobi mahali ambapo pia aliteuliwa kuwa Gombera. Kisha amewahi kuwa Gombera wa seminari kuu ya Falsafa ya Njiro Arusha.

Kati ya mwaka 1998 na 2004 alifanya kazi katika Halmashauri kuu ya Shirika, makao makuu huko Roma. Aliporudi nyumbani aliteuliwa kuwa paroko wa Kipawa na msimamizi wa mahakama ya kanisa Jimbo kuu la Dar es Salaam hadi 1.6.2009 alipoteuliwa kuwa Msimamizi. wa Kitume wa Jimbo la Same.

HISTORIA FUPI YA JUBILEE YA MIAKA 100 YA UINJILISHAJI JIMBO LA SAME
 
Jimbo la Same, lenye ukubwa wa kilomita za Mraba 10,800, lilianza kuinjilishwa na wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu ( Holy Ghost/Spiritan Fathers ) mwanzoni mwa Karne ya 20, wakati Parokia Mama ya Jimbo ya Mt. Odilia Kilomeni, iliposiwa mbegu ya kwanza ya umisionari katika eneo hilo la uwanda wa milima ya Upare.

Uinjilishaji wa Mashariki mwa Afrika

Wamisionari Wakatoliki wa kwanza kufika kuinjilisha rasmi eneo la Mashariki ya Afrika, walikuwa wa shirika la Roho Mtakatifu toka provinsia ya Ufaransa. Asili ya shirika hilo ni muunganiko wa shirika lililoanzishwa na Pd. Claude Francis Poullart des Places na lile la Moyo Mtakatifu wa Maria lililoanzishwa na Pd. Francis Maria Paul Liberman . Kwa vile walikuwa na lengo moja la kuwahudumia wafanyakazi na watumwa maskini wa Afrika, waliamua kuungana wakaanzisha Shirika la Roho Mtakatifu ( Holy Ghost/Spiritan ) siku ya Pentekoste Juni 10, 1848, na Pd. Liberman akawa mkuu wao wa kwanza. Walielekeza utume wao kwenye makoloni ya Wafaransa ya Reunion , Guinea , Mauritius , na Haiti .

Hata hivyo Pd. Armand Fava toka Reunion ndiye alianza kuwasili Zanzibar mnamo Desemba 22,1860, akiwa na mapadri wawili, masista sita, tabibu wa Jeshi la majini la Kifaransa na wasaidizi wengine na kuanza makazi Zanzibar . Mwaka huo (1890) Papa Pio IX aliridhia kuanzishwa Prefecture ya Kitume ya Zanguebar ambayo ingeenea toka rasi ya Guardaful (pembe ya Afrika) hadi ilipo Msumbiji sasa, chini ya Askofu Maupoint wa Reunion , ambaye aliwaomba Shirika la Roho Mtakatifu waje kuinjilisha eneo hilo .

Juni 1863, mapadri wa Roho Mtakatifu – Antony Horner na Edward Baur (Père Ettiene) – na mabruda Celestine Cansot na Felician Gruneisen, walifika Zanzibar wakitokea Alsace . Wakati huo Zanzibar ilikuwa na soko kubwa la watumwa kuliko yote duniani.
 
Mnamo Machi 1968 walifika pwani ya bara na kuanzisha rasmi misheni ya Bagamoyo kama lango la kuendeleza uinjilishaji mashariki mwa Afrika. Pd. Horner alifanywa Makamu Msimamizi wa Kitume wa Prefecture ya Zanguebar, akifuatiwa na P. Ettien mwaka 1880, na kisha Jean Marie Raoul de Courmont kuanzia1883 hadi 1896.
 
BAADA ya majaribio kadhaa ya kuinjilisha pwani ya karibu , walianza kupenya ndani (bara). Hivyo Julai 1890, Askofu J. M. Raoul de Courmont na mapadri Augustin Commenginger na Alexander Le Roy, waliondoka Bagamoyo wakipitia Mombasa na Likoni, safari iliyowafikisha kwenye milima ya Usambara na Upare mwezi Agosti 1890.

Wakianzia Pare ya kusini walipitia Gonja na kukaa Kisiwani siku mbili kwa vile baadhi ya wapagazi walitoka eneo hilo . Waliendelea hadi Usangi na Ugweno tarehe 8 Agosti wakafika ziwa Jipe. Walipitia njia ya Taveta (Kenya), na tarehe 15 Agosti wakiwa tayari eneo la Kilimanjaro waliadhimisha Misa ya Kupalizwa Bikira Maria, ndipo kesho yake wakafika Kilema kwa Mangi Pfumba ambamo baadaye walianzisha misheni ya kwanza hapo.

Mwaka 1892, Askofu De Courmont alifanya safari nyingine kupitia Voi (Kenya), huko akaanzisha misheni za Bura (1892), ikifuatiwa na Kibosho (1893), na baadaye zikaanzishwa za Nairobi (1899), Mlingano (1902), Kondoa Irangi (1907), Galappo (1908) na Kilomeni (1909) ambayo ni misheni ya kwanza eneo la Upare.
 
Kiuongozi, tayari mwaka 1906 Vikarieti (Jimbo changa) ya Bagamoyo iliundwa na kutenganishwa na ile ya Zanguebar na Padri Francois-Xavier Vogt akawa Askofu wake tokea 1906 hadi 1923. Mwaka 1910 Vikarieti ya Bagamoyo nayo iligawanywa na kuzaa vikarieti mpya ya Kilimanjaro chini ya Askofu Marie Joseph Aloyce Munsch kama Msimamizi wake wa Kitume wa kwanza tokea 1910 hadi 1923.
 

Home | About | NewsSitemap | Contact

Copyright ©2015 www.dioceseofsame.org. Powered by

Contact Us

DIOCESE OF SAME
P.O. Box 8,
SAME
Tel: 00255-27 2758028
E-mail: [email protected]